Wednesday, November 21, 2012

Mjasiriamali anapaswa kujifunza mambo mapya


LEO nitazungumzia  dhana ya ujasiriamali kwamba ni mchakato wa kujifunza.Ujasiriamali hauna mwisho  na ni mchakato wa kujifunza. Hoja hii inathibitishwa na ukweli kwamba mabilionea ulimwenguni walianza hatua ya chini,  wakafanyia kazi mapungufu yao na kuweka mikakati ya mafanikio ya  hapo walipo leo.

Tunaposema ujasiriamali ni mchakato wa kujifunza tuna maana unapofanya biashara kuna mambo mengi unajifunza na kugundua, kuna milima na mabonde umepitia na kufika ulipo leo.

Pamoja na kukutana na vikwazo vya hapa na pale, wajasiriamali bado wana ari ya kuendelea mbele ili wanikiwe zaidi na zaidi. Kitalaam, mchakato wa kujifunza katika ujasiriamali unahusisha namna na uwezo wa kuona fursa ambazo wengine hawazioni na kubadilisha mfumo wa kufanya biashara kizamani na kuwa wa kisasa ambao unazingatia taratibu na maadili ya biashara husika.

Kubadilisha mfumo wa kufanya biashara na kugundua fursa za biashara, yote hayo hayaji kirahisi bali yanatokana na  juhudi binafsi za kutafuta habari na taarifa kupitia vyanzo tofauti.

Moja ya njia za kupata taarifa ni kupata mafunzo, kujisomea vitabu na maandiko mbalimbali kuhusu biashara husika.

Pia mjasiriamani anaweza kupata taarifa kwa njia ya kusafiri na kuona wengine wanafanya nini na kuzungumza na  wajasiriamali waliofanikiwa kuliko wewe. Tumeshuhudia mjasirimali anaanza na biashara A na baada ya muda anakua ameshafikia biashara B na zaidi, yaweza kuwa ni mwendelezo wa ukuaji wa ile ile biashara A au ni baishara nyingine kabisa baada ya biashara A kufa.

Kimsingi wakati mwingine tunajifunza kupitia makosa na uzoefu, yawezekana ulikosea mwanzoni unapoanza biashara au ulikuwa na mapungufu kwa mfano, mtaji mdogo, ujuzi hafifu wa biashara husika, lakini baada ya kukaa katika biashara hiyo kwa muda fulani unakuwa na uzoefu unaokupa ujasiri wa kupambanua mambo mbalimbali.

Mpendwa msomaji unapoona biashara haiendi kama unavyotegemea usikate tamaa, na kwa wewe ambaye haujaanza biashara ila una ndoto ya kumiliki biashara usiendelee kusitasita muda utakutupa mkono amua leo na anza kujipanga kuanzisha biashara. Fanya biashara ukitambua kuna mitihani na majaribu mbalimbali. Usikate tamaa ni mwiko, kila wakati hakikisha unapata uelewa mpya kuhusu mambo yote yanayoizunguka biashara yako.

No comments:

Post a Comment