Saturday, July 28, 2012

NAMNA YA KUANZISHA BIASHARA.....

Ukitaka kufanya biashara yoyote ile unatakiwa kufanya utafiti. Kutokufanya utafiti ni chanzo cha biashara nyingi kuharibika. Lazima ujiulize kwamba unataka kufanya biashara gani? Usiseme unataka kufanya biashara yoyote ile kwani kusema kwamba unataka kufanya biashara yoyote ile ni kupoteza mwelekeo kwa kuwa utakuwa hujui unataka kufanya nini. Kama hujui cha kufanya hakuna kitu utakachokifanya. Hili ni tatizo la watu wengi. Hata baadhi ya watu niliokutana nao wakitaka ushauri wamekuwa wakisumbuliwa na tatizo hili. Njia ya kukusaidia kuamua ufanye biashara gani ni kwa kujiuliza umewahi kufanya kazi au biashara gani? Umesomea nini? Vipaji vyako ni vipi? Ni biashara ipi au kazi ipi unapenda zaidi kuliko nyingine na kwa sababu gani? Ukisha jiuliza maswali haya chukua kalamu na karatasi uandike maswali yako na kuyajibu. Ukikagua maswali na majibu yako utagundua shughuli unayoipenda, unayoiweza na una kipaji nayo na hiyo ndiyo inayokufaa. Ukishachagua biashara unayoipenda ni rahisi sana kufanikiwa kwani shughuli utazifanya kwa hiyari bila kujilazimisha. Kama unashindwa kuamua ni biashara gani ufanye, soma sura ya sita katika kitabu hiki. Nimeelezea kuhusu mawazo yanayoweza kukusaidia kuanzisha biashara mbalimbali ambazo unaweza kuzifanya. Kama utakuwa bado hujafikia uamuzi baada ya hapo basi tafuta na wasiliana na washauri ili mbadilishane mawazo na ufundishwe jinsi ya kuamua ufanye biashara gani.
Mambo mengine unayotakiwa kuyafanyia utafiti ni:-
(i) Kujua siri ya bishara unayotaka kufanya ili upate mbinu za kupata mafanikio. Unaweza kupata siri au kujifunza mbinu kutoka kwa watu wanaofanya biashara kama unayotaka kufanya. Suala hili ni gumu sana kwani wafanyabiashara wengi huwa wanaficha siri za biashara zao ili kulinda wasizidiwe maarifa na washindani wao. Unaweza kuipata siri hiyo kama utakwenda kupata ushauri toka kwa mfanyabiashara ambaye yuko mbali na mahali unapofanyia biashara, au tafuta ushauri kwa wataalamu wa mambo ya biashara.
(ii) Fanya utafiti wa soko la bidhaa unazouza au unazotarajia kuuza. Jiulize, je bidhaa unazotaka kuziuza zina soko? Utawauzia watu gani na utauzaje? Kama wewe ni mzalishaji, una mazao / bidhaa unapaswa kuuza kwa jumla, mchanganyiko ama rejareja? Je utatangaza vipi bidhaa zako? Maelezo ya namna ya kutangaza bidhaa zako utayapata katika Sehemu ya Tatu ya Kitabu hiki. Utafiti wa soko unaweza kuufanya kwa kuwauliza wafanya biashara waliotangulia maswali hayo ya utafiti kwani wao wamekuwapo kwenye soko na wanazijua siri za soko.
(iii) Tengeneza bajeti yako kwa kuorodhesha vitu vinavyohitajika na gharama zake ili kuweza kuanzisha biashara yako. Vitu hivyo ni:-
(a) Gharama za Kujenga au kupanga ofisi
(b) Gharama za Leseni ya biashara
(c) Makadirio ya kodi toka TRA
(d) Garama ya vifaa vya ofisi yaani, Samani, makaratasi, mitambo, mashine, nk
(e) Manunuzi ya malighafi au bidhaa za kuanzia biashara
(f) Idadi ya wafanyakazi na gharama za mishahara yao.
(g) Gharama nyinginezo kama vile, umeme, maji, nk.
(iv) Unatakiwa kujua ni mtaji kiasi gani unahitajika kuanzisha biashara yako. Mtaji huo utaujua baada ya kujumlisha gharama zilizoorodheshwa katika kupengele namba (iii)Gharama hizi ni za mwaka ule wa kwanza wa kuanzia
(v) Tafuta Mtaji.
Mtaji unaweza kupatikana kutoka kwenye vyanzo vifuatavyo:-
(a) Akiba au mshahara
(b) Msaada au mkopo kutoka kwa ndugu na jamaa.
(c) Kuingia ubia na mtu mwenye mtaji
(d) Mkopo toka baadhi ya asasi kama vyama vya akiba na mikopo (SACCOS), NGO za kifedha sipokuwa Benki kwani hizi huwa hazitoi mikopo kwa mtu anayeanzisha biashara.

TARATIBU ZA KISHERIA ZA KUFUATA ILI KUANZISHA BIASHARA

Baada ya kufanya utafiti na kupanga mipango ya kuanzisha biashara unatakiwa kwanza kuangalia taratibu za kisheria ambazo unatakiwa kuzifuata na kuzitekeleza. Kama biashara yako ni ndogo anza kama mtu binafsi. Faida ya kuanza biashara kama mtu binafsi ni urahisi wa kuanzisha biashara; urahisi na wepesi wa kutoa maamuzi kwani huhitaji ridhaa ya mtu mwingine kabla ya kutoa uamuzi; mtaji unaohitajika utakuwa mdogo kutokana na gharama za uendeshaji kuwa ndogo, biashara hii inaweza kuendeshwa kwa msaada wa familia kwa kumtumia mke au mume, watoto au ndugu na jamaa na raslimali za familia kama nyumba na samani. Unapoanzisha biashara na kuiendesha mwenyewe unakuwa huru tofauti na mifumo mingine. Matatizo ya kufanya biashara kama mtu binafsi ni:- Kushindwa kupanua biashara yako kwa ufinyu wa mtaji; kufilisiwa mali zako za binafsi iwapo biashara yako itafilisika kwani katika mfumo huu mali ya biashara na mali binafsi si rahisi kuzitenganisha; Kuongeza mtaji inakuwa ni vigumu, hivyo unaweza kushindwa kupanua biashara yako. Ili kuepukana na matatizo niliyoyataja hapo juu unaweza kuungana na watu wengine kufanya biashara kwa ubia. Faida za kufanya biashara kwa ubia ni: Kupata fursa ya kuongeza mtaji kwa kushirikiana na wafanyabiashara wengine ambao wataleta mitaji yao; Kuongeza ujuzi katika shughuli kwa kuleta wataalamu pale taaluma Fulani inapohitajika. Matatizo ya kuendesha biashara kwa njia ya ubia ni: Kufilisiwa mali zako binafsi endapo biashara yako itafilisika; kudhulumiana mali endapo moja wa wabia atakuwa si mwaminifu ambapo anaweza kuingia mikataba mibovu na kusababisha hasara ambayo itabebwa na wabia wote. Ni muhimu kuwachunguza watu tunaotaka kujiunga nao ili tujue kama ni waaminifu. Pia ni vyema kuwapo na mkataba wa maandishi mnapoanzisha biashara ya ubia mkimshirikisha mwanasheria kama shahidi ili kujikinga na kudhulumiana; Kufariki kwa mbia mmoja kunaweza kusababisha kuvunjika kwa ubia; kotokuelewana kwa wabia kunaweza kusababisha kuvunjika kwa ubia. Kama biashara ikikua unaweza kuanzisha kampuni. Mfumo wa uendeshaji wa kampuni unazo faida zifuatazo: unatenganisha majukumu ya wamiliki mali na kampuni yaani kampuni inaposajiliwa inakuwa inakuwa na hadhi na kutambulika kisheria kama ni mfumo tofauti na wamiliki. Mfumo huu unatenganisha majukumu kati ya menejimenti na wamiliki wa kampuni; madeni ya kampuni yatalipwa hadi kufikia kikomo cha mtaji uliowekezwa na wamiliki. Hivyo, mali binafsi za wamiliki wa kampuni haziwezi kukamatwa kufidia madeni ya kampuni endapo kampuni itafilisika. Mfumo wa kampuni unatoa nafasi ya kupanua mtaji kwa kukusanya mitaji kwa kuongeza wanahisa au kupitia soko la mitaji ya hisa. Mfumo huu ndiyo unafaa kwa biashara kubwa kwani unatoa nafasi ya kupanuka kwa biashara na kuendelea kuwapo kwa biashara hata kama baadhi ya wamiliki wake wakifa au kujitoa katika kampuni.

Mambo ya muhimu ya kutekeleza kisheria kabla ya kuanzisha biashara ni:-


(a) Kuwa na ofisi
(b) Kukata leseni
(c) Kusajiliwa na TRA kama mlipokodi na kupewa namba ya mlipakodi
(d) Kufanyiwa makadirio ya kodi ya mapato ya awali
(e) Kutimiza masharti mengine ya keshiria kuwa mfano kama wewe unataka kufanya biashara ya ukandarasi wa ujenzi wa majengo lazima usajiliwe kwenye Bodi ya Wakandarasi.

Kama unafanya biashara ya kati au kubwa unapaswa kufuata sheria. Ni makosa kufanya biashara bila kufuata sheria za nchi. Hata hivyo, kuna biashara zingine ndogo ndogo sana kiasi kwamba uanzishaji wake si rahisi kufuata sheria hizo hapo juu, mfano uuzaji wa maandazi, karanga na vitu vingine vidogovidogo. Hizi zinaitwa biashara zisizo rasmi au biashara ndogondogo. Ni vyema ukachunguza kama biashara unayoifanya ni ndogo au kubwa ili ujue kama unapaswa kufuata taratibu za kisheria au la, kwani kutokujua utaratibu na sheria siyo kinga ya kukufanya usishitakiwe.



Tuesday, July 10, 2012

UJASIRIAMALI---UFUGAJI BORA WA KUKU WA KIENYEJI


Idadi ya wanyama wanaofugwa kwa chakula imezidi ile ya binadamu zaidi ya mara mbili kote ulimwenguni. Kuna maelfu ya wanyama kote duniani ilihali ni wachache tu wanaoweza kufugwa. Kati ya hawa wanyama, ni aina nne (Ng'ombe, kondoo, mbuzi na kuku) wanaochukua asilimia 95% ya wanyama wote wanaofugwa. Wanyama hawa hupatikana katika nchi za hari kwenye nyanda za chini. Lakini kati ya mifugo hawa, kuku ni maarufu katika nchi za hari na hata kote ulimwenguni.

Lengo la makala haya ni kutoa maelezo ili kusaidia wafugaji wa kiwango kidogo katika nchi
zinazostawi, katika kupunguza umaskini. Sehemu ya kwanza (I) itatoa maelezo kuhusu ufugaji na hasa ufugaji wa kuku, Sehemu ya pili (II) itaangazia maswala yafuatayo katika kuinua hali ya uchumi kwa kufuga kuku:

1. Kuendeleza ufugaji wa kuku za kienyeji kwa kutumia njia zisizohitaji gharama nyingi.
2. Kutafuta mbinu na njia muafaka za kuzalisha viwango vya kuku bora kwa njia ya kiasili.
3. Matumizi ya njia za kiasili au zile zisizo gharimu pesa nyingi kutibu na kuzuia magonjwa ya kuku.

SEHEMU YA I: MAELEZO KUHUSU UFUGAJI WA KUKU KATIKA NCHI ZINAZOENDELEA

NAFASI YA MIFUGO
Licha ya kukosa mashamba makubwa ya kuendeleza ufugaji wa ng'ombe, jamii nyingi katika nchi za hari (tropics) hupata nafasi ya kufuga kuku kwa kiwango kidogo.

Idadi ya wanyama wanaofugwa huongezeka sambamba na ile ya watu. Idadi ya watu inapoongezeka ndipo ile ya mifugo huzidi.

Idadi kubwa ya watu huhitaji chakula kingi na matumizi huongezeka, hivyo basi watu hufanya bidii kuzalisha chakula na mapato kutoka kwa shamba.

Ufugaji wa ng'ombe na wanyama wanaohitaji lishe kwa wingi huhitaji kiasi kikubwa cha shamba ili kupanda mimea na lishe la mifugo. Ukilinganisha na ufugaji wa kuku, utahitaji mabaki ya vyakula na sehemu ndogo ya shamba. Ufugaji wa kuku umeweza kunawiri hata pasipo fedha.

Katika nchi za hari ufugaji wa kienyeji hautahitaji kazi nyingi, kazi hii hufanywa na akina mama na watoto. Kwa kawaida katika nchi hizi kazi nyingi za nyumbani hutekelezwa na mama. Vyakula vya kuku vyaweza kutoka kwa: 1) Mabaki ya chakula, 2) Mabaki ya mimea, 3) Mabaki kutoka jikoni na 4) Vyakula vya kujitafutia (kwa mfano kwekwe, mbegu, wadudu, nyongonyongo, n.k).

Mfumo wa kufuga kuku kwa njia ya kienyeji hutumia viungo vinavyopatikana kwa urahisi na kuimarisha hali ya kiuchumi na chakula bora kwa jamii.

Ni muhimu sana kufuga mifugo hata ikiwa ni kwa kiwango kidogo kwa sababu ya 1) Chakula bora na kuongeza mapato ya jamii kwa viwango vya kuridhisha; 2) Mifugo ni hakiba au banki, faida yakehuzaana tu kama riba ya benki; 3) Mifugo yaweza kuuzwa ili kugharamia karo ya wanafunzi,malipo ya hospitali, gharama nyingine za nyumbani na hata shambani; 4) Kwa matumizi ya kijamii (kwa mfano kulipia mahari, shughuli za kidini, n.k); 5) Mifugo husaidia katika kukabili wadudu,kwekwe na kuimarisha rutuba kutokana na mbolea ya kinyesi. Ni bayana kwamba mifugo ni muhimu sana kwa mkulima yeyote yule.

UMUHIMU WA UFUGAJI WA NJIA YA KIENYEJI
Ufugaji wa kuku katika nchi zinazostawi waweza kugawanywa mara mbili: 1) Ufugaji wa
kitamaduni au kienyeji pasipo kuwepo gharama, na 2) Ufugaji wa kisasa unaohitaji fedha nyingi.

Ufugaji wa viwango vikubwa kwa kuzingatia mfumo wa kisasa ni maarufu katika kuzalisha kuku wa nyama na wale wa mayai. Mfumo huu hujumuisha asilimia ndogo sana ya aina ya ufugaji.

Itafahamika kwamba mfumo wa kisasa haujaadhiri ule wa kienyeji. Idadi kubwa ya watu katika nchi za hari hutegemea mfumo wa kienyeji kwa nyama na mayai.

Mfumo wa kisasa huhitaji pesa nyingi za kununua vyakula vya kuku. Aidha mfumo wa kisasa huhitaji kazi nyingi ili kutekeleza. Mfumo wa kisasa umefaulu katika nchi zilizostawi kutokana na hali nzuri ya kiuchumi katika kuzalisha (kuku wa hali ya juu, kuangua vifaranga kwa stima, vyakula vilivyo na madini mengi, vifaa na zana za mashine,utaalamu wa hali ya juu n.k). Haitafaa sana kuanzisha mfumo kama huu katika vijiji vya mataifa yanayostawi.

"Mageuzi" katika ufugaji (kuambatanisha mfumo wa kisasa pamoja na ule wa kienyeji) yamefanyiwa majaribio katika mataifa yanayostawi tangu miaka ya 1950.

Matokeo ya kuku wapatao 200 hadi 300kwa shamba moja hayajawai kufaulu. Hasara imepatikana na waweza kuona nyumba zilizokuwa na kuku bila chochote, pesa nyingi zimepotea na kuku hawapo.

Mfumo wa kienyeji ni bora (Katika hali ya kiuchumi) iwapo idadi ya kuku haitazidi kuku 50. Ni rahisi kuweza kuwatunza kuku, kwani hakuna gharama nyingi. Iwapo vyakula au zana za kisasa zitanunuliwa, basi haitakuwa kwa viwango vikubwa. Mazao ya nyama na mayai yataleta faida.

Sehemu nyingi katika mataifa yanayostawi hakuna stima, katika nchi za hari, ufugaji kwa kiwangokidogo umeweza kufaulu na kuimarisha uchumi.

FAIDA ZA UFUGAJI WA KUKU KWA NJIA YA KIENYEJI
Faida za uzalishaji kuku ili kuimarisha uchumi kwa njia hii zimepuuzwa na viongozi na wafadhili.

Kuku huleta faida kwa jamii kama tulivyoona katika sehemu ya I. Zaidi ya hayo, ufugaji wa kuku waweza kuimarishwa pasipo gharama nyingi ukilinganisha na mifugo wengine.
· Hutupatia fedha kwa kuuza nyama na mayai
· Mayai ni chakula kilicho na madini muhimu na kisicho ghali katika soko lolote. (madini kama methionine na cystine), madini haya ni muhimu sana kwa afya ya watu hasa watoto wachanga. Pia hutupatia protini.
· Kinyesi cha kuku ni mbolea safi
· Kiwanda asilia cha kutotoa vifaranga
· Gharama za kuanzisha na kuendeleza ni nyepesi
· Kitoweo chepesi na rahisi kwa wageni, kitoweo hakihitaji hifadhi hutumika mlo mmoja au miwili na kumalizika
· Jogoo hutumika kama saa inapowika
· Manyoya ya kuku hutumika kutengenezwa mapambo mbalimbali, mito na magodoro
· Kuku wanahisimu wadudu waharibifu

Kuku ndiye mnyama wa kipekee anayeweza kuishi mahali popote hapa ulimwenguni bila kuadhiriwa
na viwango vya hali ya hewa. Ufugaji wa kuku ndio shughuli inayofanyika kwa wingi duniani kuliko ufugaji wa aina yeyote. Kuku hunawiri vyema katika nchi za hari kutokana na uwiano uliopatikana wakati wa mwanzo binadamu alipofuga Asian jungle fowl aina ya kuku-mwitu. Mayai pia yaweza kuhifadhiwa kwa urahisi na huchukua nafasi ndogo kuliko aina ya bidhaa zozote za mifugo. Mayai yaweza kuwekwa mahali kwa muda mrefu bila kuhitaji barafu. Hautahitaji kuhifadhi kuku kwa njia yoyote, kwani nyama yake hupatikana pale unapohitaji kwa kuchinja.
Upungufu wa kuku wa kigeni ukilinganisha na wale wa kienyeji ni kama ufuatao:
• Kuku wa kigeni hawawezi kukalia na kuangua mayai, hivyo basi wahitajika kununua vifaranga (gharama);
• Vifaranga wa kigeni huhitaji utunzaji maalum na vyakula maalum (gharama);
• Kuku waliozalishwa kwa njia ya kisasa huhitaji chakula kingi ili kutaga mayai (gharama);
• Kuku wa kisasa huhitaji zaidi kuchanjwa dhidi ya magonjwa (gharama)ukilinganisha na wa kienyeji (japo nao huhitaji chanjo);
• Kuku wa kutaga mayai huhitaji mwangaza wa stima (saa 14 kwa siku) ili kutaga mayai (gharama)
Kwa kuongezea, rangi ya nyama na mayai ya kuku wa kienyeji huvutia kuliko ile ya kuku wa kisasa.
Hivyo basi jaribu kuendeleza na kuhimiza ufugaji wa kuku wa kienyeji.
Iwapo mkulima ana jogoo mmoja na kuku kumi na mbili, basi kila mwezi waweza kupata kuku akikalia mayai 10-12 kwa mwezi (mayai yote kwa wakati mwingi hayataanguliwa) kuna hakikisho la kupata vifaranga vinne kila mwezi. Kuku mzima atachukua miezi minne kuchunga vifaranga walioanguliwa.

Kwa hivyo, kati ya kuku wote kumi na mbili kila mara kutakuwa na kuku wanne wakitunza vifaranga, huku wale wengine wanane wakitaga mayai.

Kuku waliofugwa kwa njia ya kitamaduni hupata vyakula vyao kwa kutafuta mbegu, wadudu
nyongonyongo, n.k; Lakini kuku hawa hukosa vyakula vya kutosha vilivyo na nguvu ili waweze kutaga mayai. Vyakula vya kutoa nguvu daima huwa ni haba.

Waweza kuwalisha kuku kwa nafaka ili wapate chakula cha nguvu (mfano kilo moja ya nafaka iliyopondwa kila siku kwa kuku 10), nafaka hii yapaswa kuwa kavu. Vifaranga wapewe kiasi kidogo cha nafaka au mchele wiki za kwanza. Kuku wanaolishwa nafaka baada ya kujitafutia chakula nje huongeza idadi ya mayai (kutoka asilimia 20-25% hadi 40-50%). Kuna umuhimu wa kuhifadhi nafaka kama lishe badala ya kuuza kwani utapata mayai mengi ambayo baadaye utaweza kuuza.

Hautahitaji kununua vyakula vya protini kwani kuku hujitafutia lishe la protini.
Ikiwa hauna nafaka, waweza kutumia vyakula vya mzizi au ndizi. Vyakula vya aina hii hata hivyo, huwatatiza kuku wanapovitonogoa, kiwango cha mayai sio kikubwa kama cha wale wanaolishwa nafaka.

Kwa kuwalisha kuku kwa nafaka utapata hakikisho la mayai manne kwa siku kutoka kwa wale kuku wanane. Iwapo hakuna nafaka, kati ya kuku wanane wanaotaga utapata mayai mawili tu kwa siku.

Ni bora kutumia nafaka hii kama lishe kuliko kuuza na hatimaye kununua vyakula vya dukani.

Kuku kumi na mbili na jogoo mmoja wanaolishwa kwa kilo moja ya nafaka kila siku waweza
kuelezwa hivi:
• Waweza kuuza kuku wanne kila mwezi na kujaza pengo hilo na wale vifaranga (vifaranga
wanne huanguliwa kila mwezi) na
• Dazani kumi za mayai kila mwezi (mayai manne kila siku).
Kwa mwaka mmoja waweza kukadiri ile faida utakayopata na vile hali ya kiuchumi yaweza
kuinuliwa katika mataifa yanayostawi.
Hata hivyo faida hii haitaafikiwa iwapo magonjwa
hayatazuiwa au kukabiliwa kama ifuatavyo.

TEKELEZA UTARATIBU WA KUZUIA MAGONJWA

Magonjwa ndio husababisha hasara katika mfumo wa ufugaji wa kuku. Kuku waliochanjwa dhidi ya magonjwa hudumisha afya bora. Jaribu kila mara kuzuia magonjwa, kwani kuzuia ni bora kuliko kuponya. Kinga yaweza kutolewa mara kwa mara (kila baada ya miezi mitatu) dhidi ya magonjwa yafuatayo:

Ugonjwa wa Newcastle
Ugonjwa huu ndio huadhiri kuku na kusababisha hasara katika nchi za hari. Virusi vya ugonjwa huu huenea kwa kasi na rahisi kiasi cha kusababisha vifo kwa asilimia 100%. Dalili za kwanza ni shida ya kupumua na kung'amua hewa, sauti kama ya kikohozi na kutokwa mate. Kinyesi chaweza kuwa na rangi ya kijani kibichi. Hadi sasa hakuna dawa.

Waweza kuzuia ugonjwa huu kwa kutoa chanjo. Dawa za chanjo hupatikana kote ulimwenguni hata katika nchi za hari kwenye vipimo vya vitone mia moja. Madawa haya yaweza kuhifadhiwa kwa muda. Waweza kuweka kwa wiki moja mbali na jua au joto kali (Chanjo hii ni ya kipekee, kwani aina nyingine ya chanjo huwekwa kwa friji). Waweza kutoa chanjo kwa kutia vitone kwenye mdomo. Kuku wote (wakubwa kwa wadogo) wapaswa kupewa chanjo baada ya kila miezi mitatu.

Minyoo
Minyoo kama chango (roundworms) na tegu (tapeworms) huadhiri kuku wa kienyeji. Kuku hukosa hamu ya chakula, mayai hupungua na magonjwa mengine hushambulia. Ni bora basi kutoa minyoo.

Mchanganyiko wa madawa ya aina tatu ndio hutumiwa kuangamiza minyoo, madawa haya ni piperazine, phenothiazine na butynorate. Madawa haya hupatikana kama vidonge (tumia kidonge 1 kwa kuku mzima na 1/2 kwa vifaranga). Iwapo hautapata dawa hii, waweza kutumia Panacur au dawa nyingine ya kuangamiza minyoo. Wapatie kuku dawa ya minyoo kila baada ya miezi mitatu.
Wadudu
Wadudu kama chawa au utitiri husumbua kuku katika ufugaji wa kienyeji. Chawa au utitiri
husababisha harara ya ngozi, kuku walio adhiriwa hupata shida na kukosa usingizi. Hali hii
hupunguza kiwango cha mayai na uzito wa kuku.

Tumia asilimia 5% ya unga wa malathion kwa kupulizia kuku (puliza kwa chupa uliyo toboa
mashimo) pulizia kila kuku ili kuzuia chawa na utitiri (kilo moja ya unga huu yaweza kutibu kuku 150). Pulizia dawa hii baada ya kila miezi mitatu, waweza kupuliza kwa wakati mmoja wa kutoa chanjo na dawa zilizotajwa hapo juu. Puliza unga huu pia kwenye viota vya kuangulia mayai.

Waweza kutayarisha 5% ya malathion kwa kuchanganya 25% ya unga wa malathion (kiwango cha kilimo) na sehemu nne za jivu kutoka jikoni.
Magonjwa ya mapafu
Magonjwa ya mapafu huadhiri njia inayopitisha hewa na kuambatanisha mate na sauti kama ya kikohozi. Ugonjwa huu huenea polepole. Uambukizanaji pia hutokea kwa polepole na vifo sio kwa wingi.

Hata hivyo, kutaga mayai na uzito hupungua. Shida hii yaweza kusambaa hata kutoka mahali vifaranga huanguliwa hadi pale walipouzwa.

Tylosin19 ndio dawa inayoweza kutibu magonjwa ya mapafu. Kiasi cha 35mg ya tylosin hutosha kuku mmoja (kiwango hiki hufaa kuku na hata vifaranga) dawa hii husimamisha madhara kutokana na magonjwa ya mapafu.

Tibu kuku kila baada ya miezi mitatu, waweza kutekeleza kwa wakatimmoja wa kutoa kinga na kuangamiza minyoo. Tylosin hupatikana kwa pakiti ndogo ya 4gm.
Waweza kutayarisha dawa hii kwa kutumia maji na 35gm ya tylosin (gramu nne kwa vikombe viwili vya maji), kiasi hiki chaweza kutolewa kwa vitone kwa kila kuku.
KWA UFUPI (SUMMARY)
Kabila za Kuku
Si rahisi kupata kabila halisi (pure breed) au kizazi halisi (pure line) za kuku wa kienyeji kutokana na mwingiliano wa vizazi kati ya aina mbalimbali za kuku hao. Lakini hata hivyo baadhi ya kuku wa kienyeji wanaweza kutambuliwa kutokana na maumbile yao kwa mfano
1. Kuchi
  • Warefuna wenye kusimama mgongo ukiwa wima
  • Wana manyoya machache mwilini na vilemba vyao ni vidogo
  • Majogoo huwa na wastani wa kilo 2.5 na mitetea kilo 1.8
  • Mayai gram 45
2. Ching'wekwe (Umbo dogo)
  • Hupatikana zaidi Morogoro na umasaini
  • Majogoo kilo 1.6
  • Mitetea kilo 1.2
  • Yai gram 37
  • kuku hawa wanafaa sana kwa biashara ya mayai kwa kuwa hutaga mayai mengi sana.
3. Umbo la Kati
  • Majogoo kilo 1.9
  • Mitetea kilo 1.1
  • Mayai gramu 43
  • Hukua upesi na hupata kinga upesi baada ya kuwachanja dhidi ya ugonjwa wa Mdondo (New Castle)
4. Singamagazi
  • Hupatikana zaidi Tabora
  • Majogoo wana rangi ya moto na mitetea rangi ya nyuki
  • Majogoo kilo 2.9
  • Mitetea kilo 2
  • Mayai gramu 56
5. Mbeya
  • Wanapatikana Ileje Mbeya na asili yao ni Malawi
  • Mjogoo kilo 3
  • Mitetea kilo 2
  • Mayai gramu 49
  • Uwezo wao wa kuatamia mayai na kuangua ni mdogo sana ukilinganisha na kuku wengine
6. Pemba
  • Maumbo ya wastani na miili myembamba
  • majogoo kilo 1.5
  • mitetea kilo 1
  • mayai gramu 42
7. Unguja
  • Hawatofautiani sana na wa Pemba
  • Vilemba vyake ni mchanganyiko- vidogo an vikubwa
  • Majogoo kilo 1.6
  • Mitetea kilo 1.2
  • Mayai gramu 42
SIFA WA KUKU WA KIENYEJI
  1. Wastahimilivu wa Magonjwa
  2. Wana uwezo wa kujitafutia chakula
  3. Huatamia, kutotoa na kulea vifaranga
  4. Wanastahimili mazingira magumu(ukame, baridi n.k)
  5. Nyama yake ina ladha nzuri
KATIKA KUWAENDELEZA KUKU WA KIENYEJI NI VYEMA
  1. Wajengewe nyumba bora
  2. Wapewe kinga dhidi ya ugonjwa wa Mdondo (New Castle), Ndui (Fowl Pox) pamoja na kinga ya minyoo.
  3. Malezi bora ya vifaranga
  4. Kuwapatia chakula cha ziada pamoja na maji ya kunywa ya kutosha.
NYUMBA BORA
Eneo inapojengwa nyumba au banda la kuku liwe
  • Linafikika kwa urahisi
  • Limeinuka juu pasituame maji
  • Pasiwe na pepo zinazovuma
Vifaa kama miti, nyasi, makuti, fito, udongo mabanzi ya miti, cement, mabati n.k
Sifa za Nyumba Bora ya Kuku
  • Paa imara lisilovuja
  • Kuta zisiwe na nyufa
  • Sakafu isiwe na nyufa
  • Madirisha ya kutosha kupitisha hewa
  • Iwe na mlango wa kuingia kufanya usafi
  • Iwe na ukubwa (nafasi) unaolingana na idadi ya kuku. Wastani wa kuku 10-15 kwa mita moja mraba
Mambo muhimu ndani ya nyumba
  • Chaga za kulalia kuku
  • Sakafu iwekwe maranda (wood shavings), makapi ya mpunga, n.k
  • Viota vya kutagia mayai sentimita 35x35x35 na idadi ya viota iwe nusu ya idadi ya kuku waliofikia hatua ya kutaga na viwekwe sehemu iliyojificha (faragha)
UATAMIAJI WA MAYAI
Kuna njia 2
  • Njia ya kubuni (incubators)
  • Asili
Kumuandaa kuku anayeatamia
  • Weka maranda au majani makavu ndani ya kiota
  • Anapokaribia kuatamia toa mayai ndani ya kiota pamoja na maranda, hakikisha mikono haina manukato
  • Nyunyiza dawa ya kuua wadudu (viroboto, utitiri n.k) ndani ya kiota, pia mnyunyizie dawa kuku anayetarajia kulalia mayai
  • Rudisha mayai kwenye kiota ili kuku aanze kuatamia
  • Kwa kawaida kuku hulalia mayai yake kwa muda wa siku 21 ndipo huanguliwa
ULEAJI WA VIFARANGA
Kuna njia mbili
  • Njia ya kubuni
  • Njia ya asili
Njia ya ASILI

Kuku mwenyewe hutembea na vifaranga akivisaidia kutafuta chakula. Ni vizuri kumtenga kuku mwenye vifaranga katika chumba chake pekee ili vifaranga wasishambuliwe na kuku wengine hali kadhalika kuwalinda na wanyama na ndege wanaoshambulia vifaranga.

Njia ya KUBUNI

Vifaranga huwekwa kwa pamoja kwenye chumba maalum na kupatiwa joto maalum, chakula pamoja na maji. Tumia taa ya kandili (chemli), umeme au jiko la mkaa na hiyo taa iweke kwenye mzingo(mduara) walipo vifaranga. Pia kuna kifaa kinaitwa Kinondoni Brooder ni kizuri kwa kutunzia vifaranga. Kwa kutumia kifaa hiki kuku wanaweza kunyang'anywa vifaranga vyao mara tu baada ya kutotoa na kuviweka kwenye hii brooder na hao kuku wakaachwa bila vifaranga vyao, baada ya majuma matatu au manne, kuku hao huanza tena utagaji na kuendelea na uatamiaji hadi kutotoa tena. Kwa mtindo huu kuku anaweza kutotoa mara 5-6 badala ya kama ilivyo sasa mara 2-3 kwa mwaka. Vifaranga vikae ndani ya brooder majuma 3-4 na baadaye fungua milango ya brooder kuruhusu vifaranga vitoke na kuzungukazunguka chumbani bila kuvitoa nje kw kipindi cha mwezi mmoja au zaidi kutegemeana na mazingira.

KULISHA KUKU WA KIENYEJI

Kuku mkubwa huhitaji gramu 120 za chakula kwa siku, ni vizuri kuku wanaofugwa huria (free range) kupatiwa chakula cha ziada gramu 30 kila siku nyakati za jioni.
Kuku walishwe
  • Mizizi-mihogo, viazi vitamu, mbatata, magimbi, n.k
  • Nafaka-mahindi, Mpunga, Mtama, Ulezi na Pumba za nafaka zote
  • Mboga-Mikundekunde, nyanya, milonge, majani ya mapapai
  • Matunda-Mapapai, maembe, n.k
  • Mbegu za Mafuta-Karanga, ufuta, mashudu ya pamba, alizeti, n.k
  • Unga wa dagaa
  • Maji
KUCHANGANYA CHAKULA CHA KUKU
  • Pumba.............kilo20
  • Mashudu ya Pamba n.k...kilo 3
  • Dagaa iliyosagwa.........kilo 1
  • Unga wa majani uliokaushwa kivulini na kusagwa........kilo 2
  • Unga wa Mifupa ..........kilo 0.25
  • Chokaa ya mifugo ........kilo 0.25
  • Chumvi........................gramu 30
  • Vichanganyio/Premix...gramu 25
KUPANDISHA
  • Uwiano wa mitetea na jogoo ni mitetea 10-12 kwa jogoo mmoja
  • Sifa za mtetea ni mkubwa kiumbo, mtagaji mayai mengi, muatamiaji mzuri na mlezi wa vifaranga
  • Sifa za jogoo ni awe mkubwa kiumbo, miguru imara na yenye nguvu, mrefu, upanga/kilemba kikubwa, awe na uwezo wa kuitia chakula mitetea na awe na tabia ya kupenda vifaranga
  • Jogoo huanza kupanda akiwa na umri wa miezi 7-10 na kuendelea hadi miaka mitatu na asipande watoto wake
  • Mitetea huanza kutaga wakiwa na miezi 6-8
MAGONJWA YA KUKU
1. Mdondo/New castle
Virus vinavyosababisha ugonjwa huu huenezwa kwa hewa
Dalili
  • Kuhalisha choo cha kijani na njano
  • Kukohoa na kupumua kwa shida
  • Kupinda shingo kwa nyuma
  • Kuficha kichwa katikati ya miguu
  • Kukosa hamu ya kula na kunywa
  • Idadi kubwa ya vifo hadi 90%
Kinga
  • Chanjo (New Castle vaccine) kwa mpango wa siku 3, wiki 3, miezi 3
  • Epuka kuingiza kuku wageni
  • Choma au fukie mizoga ya kuku waliokufa kwa ugonjwa
  • Zingatia usafi wa mazingira
NDUIYA KUKU/ FOWL POX
Virus huambukizwa kupitia jeraha au mbu
Dalili
  • Vidonda vyenye utando wa kahawia/purple kwenye sehemu zinazoonekana
  • Kukosa hamu ya kula
  • Vifo vingi
Kinga
  • Chanja vifaranga wanapofikia mwezi 1-2 kwa kutumia chanjo ya Fowl pox vaccine
  • Epuka kuingiza kuku wageni
  • Zingatia usafi wa mazingira
HOMA YA MATUMBO/FOWL TYPHOID
  • Kuharisha kinyesi cha kijani na nyeupe
  • Kuku hukosa hamu ya kula
  • Kuku hukonda
  • Vifo hutokea kidogo kidogo kwa muda mrefu
  • Kinyeshi hushikamana na manyoya
Tiba
Dawa aina ya antibiotic, sulfa na vitamini
Kinga
  • Usafi
  • Fukia mizoga
  • Usiingize kuku wageni
  • Chinja kuku wote mara ugonjwa huu ukiingia na safisha banda, pia pumzika kufuga kwa miezi 6
MAFUA YA KUKU/INFECTIOUS CORYZA
Hutokana na bakitelia na hushambulia hasa kuku wakubwa
Dalili
  • Kuvimba uso
  • Kamasizilizochanganyikana na usaha unaonuka
  • Macho huvimba na kutoa machozi na pengine upofu
  • Hukosa hamu ya kula
  • Mbawa huchafuka na kutoa harufu mbaya
Tiba
Dawa za Antibiotic, sulfa na vitamini
KUHALISHA DAMU/COCCIDIOSIS
Husababishwa na vijidudu vya Protozoa
Dalili
  • Kuharisha damu
  • Manyoya husimama
  • Hulala na kukosa hamu ya kula
MINYOO
Dalili
  • Kunya minyoo
  • Hukosa hamu ya kula
  • Hukonda au kudumaa
  • Wakati mwingine hukohoa
Tiba
Dawa ya minyoo/Pipeazine citrate kila baada ya miezi mitatu
WADUDU
Viroboto, chawa, utitiri
Dalili
  • Kujikuna na kujikung'uta
  • Manyoya kuwa hafifu
  • Rangi ya upanga kuwa hafifu
  • Ngozi kuwa nene, ngumu na yenye magamba yanayodondoka kama unga
Kuzuia
  • Ziba mipasuko sakafuni na kwenye kuta za banda
  • Fagia banda mara mbili kwa wiki
  • Nyunyiza majivu au chokaa mara moja kwa wiki mara baada ya kufagia
  • Choma masalia ya mayai yaliyoanguliwa
  • Nyunyiza dawa kwenye viota
  • Weka maranda, majani makavu, makapi ya mpunga ya kutosha sakafuni ndani ya banda la kuku
  • Fuata kanuni za chanjo
  • Tenga kuku wagonjwa wakae mbali na kuku wazima
UPUNGUFU WA VIINI LISHE KWENYE CHAKULA
Dalili
  • Kuku hupungua damu, uzito na kudumaa
  • Mifupa huwa laini na kutokuwa imara
  • Hutaga mayai yenye gamba laini na madogo
  • Huwa na manyoya dhaifu
KAZI KWENU WAFUGAJI...!!!!!!

Mfahamu Mwanamke Mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa Nchini Tanzania....


Tukizungumzia wanawake wajasiriamali wenye mafanikio makubwa nchini Tanzania,huwezi kukosa kumtaja Rita Paulsen ,Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni maarufu ya Benchmark Productions yenye makao yake makuu jijini Dar-es-salaam.

Rita ambaye ana uzoefu wa zaidi ya miaka 12 kwenye masuala ya utengenezaji matangazo na masoko,sio tu ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo yenye mafanikio nchini Tanzania na kimataifa, bali pia ni mmojawapo wa majaji katika show maarufu ijulikanayo kama Bongo Star Search. Show hiyo ambayo hivi karibuni imezidi kujipatia umaarufu mkubwa nchini Tanzania,ni ubunifu mwingine mahiri wa Rita na kampuni yake ya Benchmark Productions.

Rita anasema alianzisha Benchmark kwa sababu kwanza alikuwa anapenda sana kujiajiri na pili wakati ameanza kulikuwa hakuna production house za quality(viwango) vizuri. Aliamini ataweza kubadilisha hilo yaani to make a difference because of  her creativity and the love she has for the work she does.

 
Wanawake oyeeee....!!!!!! Juhudi zako zinaonekana Madam